Tuesday, December 15, 2015

YALIYOJIRI 2015

Tukiwa ukingoni mwa mwaka 2015 kuna watu ambao kupitia mienendo na haiba zao wamenikuza, wamenifunza na wameniwekea misingi ya kujipima kwa namna mbalimbali.
Kupitia maneno yao na matendo yao wamekua taswira ya washauri wa mbali wenye kuleta tofauti kubwa katika jamii yetu.

Watu hawa kwangu wameweka mfano wa kiwango cha juu kukitaraji ama kukifikia katika kukidhi matazamio ya utashi binafsi lakini kwa namna ambayo inajali wale wote wanaokuzunguka.

MWANASIASA WA MWAKA: SEIF SHARRIF HAMAD.

Usipoweza kuufurahia ushindi wako kwa utu, huwezi kupokea kushindwa kwako kwa utu.

Maalim Seif ni mfano wa wanasiasa wachache sana wa kiafrika ambao wameonyesha kuheshimu sana njia ya kidiplomasia katika utatuzi wa migogoro.
Ni mwanasiasa anayejiamini, mwenye msimamo na asiyetetereka lakini amedhihirisha ni kiongozi mwenye staha ya daraja ya juu na muumini wa mazungumzo ya pande mbili zinazokinzana bila kujali mizani ya haki imeegamia upande gani kabla ya shauri husika.

Maalim Seif pamoja na kuwa mshindi halali wa uchaguzi na muathirika wa uamuzi batili wa tume ya uchaguzi bado kwa juhudi binafsi amekua kinara na kichocheo cha mazungumzo ya kutafuta suluhu juu mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.

MWANAMKE WA MWAKA: MAMA REGINA LOWASA.

Mwanamke bora kwa kiasi kikubwa ndiyo chachu ya familia bora, ndoa bora na jamii bora.

Ushujaa wa sauti ya wanawake katika harakati za ukombozi zilizaliwa upya kutoka katika roho zilizopumzika za wanawake mashujaa kama Bibi Titi Mohammed na Mwamvua Mrisho (aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa umoja wa wanawake wa Tanu).
Mama Regina alikua sauti ya wanawake walio wengi bila kujali tofauti zao kiitikadi na matabaka yao.
Aliongelea changamoto za kina mama na kuwafikia wakina mama wengi ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza madukuduku yao.
Aliamsha ari kubwa miongoni mwa wanawake na kujenga ushawishi wa ushiriki wa wanawake katika siasa.

Mwaka huu alikua ni alama ng'aavu ya uwezo mkubwa wa wanawake katika kujenga ushawishi ndani ya jamii, alikua ni nuru ya wanawake katika kuzungumzia na kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii.

Alikua ni nembo ya mke anayeijenga ndoa yake kwa mikono yake, alikua ni kielelezo cha kupigiwa mfano cha mke mwema aliye msaidizi mkuu wa mume wake kama ilivyokua kwa asili ya uumbaji uliotukuka wa Mungu.

Yote haya aliyafanya bila kutetereka huku akitimiza majukumu yake vyema kama mke, mzazi, mlezi, mwalimu jamii na mwanaharakati kisiasa.

HAIBA YA MWAKA:MH EDWARD NGOYAI LOWASSA.

Kuna wakati wa kuongea na kuna wakati wa kukaa kimya, wengi ni wepesi zaidi katika kuongea na wengi zaidi ni wepesi katika kuropoka kwa msukumo wa hisia, lakini wachache sana ni wenye kujua thamani ya kukaa kimya.

Miongoni mwa wachache sana wenye kujua thamani ya kukaa kimya, sijawahi kushuhudia haiba yenye utulivu na staha ya daraja ya juu dhidi ya mihemko yenye joto kali, dhidi ya shutuma zenye kudhalilisha utu katika uasili wake, dhidi ya udhalilishwaji wenye kufedhehesha hata nafsi zilizo pembezoni....sikuwahi kushuhudia hapo kabla.

Sijawahi kushuhudia haiba yenye heshima na utu dhidi ya udhalimu na ufedhuli.
Sijawahi kushuhudia haiba yenye kupiga makasia kwa utulivu wa nafsi na akili ndani ya bahari iliyochafuka yenye mawimbi makubwa ya kuzimisha ndoto, kukatisha tamaa, kuchafua haiba, kuombewa kifo, kuwekewa maneno mdomoni, kuinuliwa vikwazo, kuvikwa nembo ya chuki....sikuwahi kushuhudia hapo kabla.

Lakini mwaka huu nimeshuhudia haiba yenye utulivu, hekima na busara kubwa dhidi ya dhoruba kali ya husda na udhalilishaji wa kupindukia , nimeyashuhudia haya katika haiba iliyosheheni staha katika kiwango cha juu cha kupigiwa mfano kutoka kwa baba yetu Edward Lowasa.

MASHUJAA WA MWAKA: WANAMABADILIKO WOTE NCHINI.

Huwezi kujua unayahitaji mabadiliko kiasi gani mpaka pale unapotambua ni mabadiliko pekee yatakayokuwezesha kujikwamua katika hali ya mtanziko na udumavu uliyopo.

Juhudi za makusudi zinazofanyika na serikali ya sasa ni muitiko wa msukumo wa sauti zilizopazwa kwa kiwango kikubwa cha utambuzi wa wanamabadiliko juu hatima na matamanio yao kama wana wa ardhi.

Kamwe tusisahau umuhimu wa nguvu ya vuguvugu la wanamabadiliko , ushujaa wao katika kupaza sauti ya mabadiliko, na ujasiri wao katika kuonyesha dhamira yao kwa vitendo, imebadili kwa kiwango cha awali (chakuridhisha) upepo wa kisiasa nchini, ikiwemo utendaji na nidhamu ya uwajibikaji.

Mabadiliko haya si utashi wa mtu binafsi au taasisi ya urais, usikosee katika tafakuri ya mantiki pana, mabadiliko haya yanaakisi kishindo kikuu cha sauti za wanamabadiliko, yanaakisi utambuzi na upevu wa fikra zilizoamshwa na wanamabadiliko.

Bila kujali matokeo ya uchaguzi nawiwa kuwatunuku heshima ya juu wanamabadiliko wote waliojitoa kwa hali na mali, kwa akili zao, nguvu zao na muda wao adhimu katika kusimamia na kukipigania kile walichokiamini.

Hakika hamkuiacha Tanzania kama ilivyokuwa awali, kupitia maono na fikra zenu nimejifunza mengi, mmetufunza wengi na hata wale waliowapuuza awali wamejifunza kimyakimya.

Hamasa huzaa matumaini, matumaini huzaa imani, imani huzaa matendo makuu.
Mabadiliko ni safari na safari ndiyo imeanza, hakika TUTAFIKA....hakika YATATIMIA.KITI CHA URAIS KITAYATIMIZA MABADILIKO TULIYOYAHITAJI NA KUYAKOSA KWA MIAKA 50.
HAKUNA NAMNA NYINGINE BALI KUYATIMIZA MABADILIKO IWE KWA KUPENDA AU KUTOKUPENDA.
2020 HAKUNA KUANGALIA USONI.

No comments:

Post a Comment